Ads 468x60px

Friday, 6 March 2015

SOMO LA LEO: UANDAAJI WA HYDROPONICS FODDER KWA AJILI YA KULISHA MIFUGO



 Hydroponics ni utaratibu wa kuotesha mimea kwa kutumia maji bila kuhusisha matumizi ya  mchanga kabisa, isipokuwa mimea inaoteshwa katika chombo maalum ‘tray” ambacho kipo katika hali ya usafi na kina matundu ya kiasi ili kusaidia maji yasituame wakati wa kumwagilizia.
 Katika somo hili tutaangalia uoteshaji wa mbegu za ngano kwa njia hii ili iweze kutumika kama chakula cha mifugo mfano: kuku, ngombe, sungura, nguruwe n.k.  Ili kuotesha mbegu zako kwa utaratibu huu utahitaji vifaa vifuatavyo:
1.       Tray ya plastiki au alminium yenye matundu ( umbo mstatili ni bora zaidi)
2.       Sprayer (chupa ya kunyunyizia maji)
3.       Mbegu za shairi au ngano (chagua mbegu ambazo hazijatobolewa na wadudu)
4.       Chombo cha kulowekea mbegu (Unaweza kutumia  ndoo yeyote)
5.       Chujio la plastiki ( Kama hauna unaweza kutumia kitambaa kisafi)
 
JINSI YA KUANDAA
1.       Pima uzito wa mbegu zako kisha zisafishe vizuri kuondoa takataka zote.
2.       Weka maji kwenye ndoo safi na kisha weka mbegu zako ili kuziloweka kwa muda wa masaa 4 au zaidi ukipenda masaa 12.Muda mrefu zaidi huwezesha mbegu kuchipua vizuri na kwa haraka.
3.       Baada ya masaa 4 au 12 kupita toa mbegu zako kwenye ndoo na uzichuje maji kwa kutumia chujio au kitambaa kisafi
4.       Baada ya kuchuja maji hamishia mbegu zako kwenye tray kisha zisambaze ili zizibanane kupita kiasi. Unaweza kutumia tray yeyote hata ungo unafaa kwa kuanzia (Mimi binafsi nilitumia ungo)
5.       Baada ya kuweka mbegu zako kwenye tray funika tray yako kwa muda wa masaa 48 (SIKU 2) tumia mfuniko wenye matundu madogo madogo na machache (Mimi nilitumia ungo mkubwa kama tray na mdogo kama mfuniko, unaweza kutumia hata ndoo kwa kutoboa matundu kiasi katika mfuniko wake. Wakati mbegu zako zipo kwenye hatua hii hakuna haja ya kumwagilia mara kwa mara isipokuwa utakagua mbegu zako na ukiona zimekuwa kavu basi utanyunyiza maji kidogo kidogo mpaka zitakapo onekana zina unyevu wa kutosha kisha endelea kufunika.
6.       Baada ya masaa 48 kupita (siku 2) mbegu zako zitakuwa zimechipua kikamilifu, utaona mfano wa nyuzi nyeupe zinachomozo.Hamishia tray zako kwenye kichanja au eneo lenye hewa ya kutosha lakini zikinge dhidi ya jua kali kwa kuweka turubai au nailoni juu ya kichanja unaweza pia kutumia hata mifuko ya unga (viloba) kutengeneza kichanja, unaweza pia kuzungusha wavu kama net za mbu ili kuzuia wadudu i.e inzi na pia kama eneo lako lina ndege wengi basi kutumia net itakuwa msaada kwako ili kuwazuia ndege hao.
UMWAGILIAJI

Mwagilia angalau mara 3 kwa siku, yaani asubuhi, mchana na jioni. Hakuna haja ya kumwagilia usiku kwa sababu hewa ya usiku huwa imepoa na kubeba unyevu wa kutosha na hata asubuhi usishangae kukuta umande kwenye fodder yako.

UVUNAJI

Unaweza kuvuna fodder yako ndani ya siku 7 au 9. Ingawaje wengine wananapendekeza kuvuna ndani ya siku ya 4 kama utalisha kuku kitu ambacho mimi sijakipendelea kwa sababu lengo la kutumia njia hii ni kuhakikisha kwamba tunapunzuza gharama ya chakula cha kuku kwa kiasi kikubwa kadri  iwezekanavyo na  iwepo utavuna kwa muda huo utapata ongezeko dogo sana mfano. Kilo 2 zitazalisha kilo 4 ya fodder wakati ukivuna baada ya siku 7 hadi 9 kilo 2 za mbegu zitazalishe kati ya kilo 12 hadi 16 za fodder.

UZOEFU:
Mimi binafsi nilinunua kilo 2 za mbegu za ngano na kuzigawanya katika ½ kilo, kisha nikazipanda katika nyungo 4 kwa maana ya ½ kilo ya mbegu kila ungo mmoja. Nilivuna fodder zangu baada ya siku ya 8 na kufanikiwa kupata kilo 16 za chakula cha kuku.
MAHITAJI YA KUKU

Mahitaji ya kila kuku mmoja ni kati ya gram 125 mpaka gram 150 za chakula kwa siku. Hivyo kilo 16 nilizozipata ni chakula cha kutosha kulisha  kuku 106 kwa siku moja ambapo nimetumia gharama ya shilingi 4,000/= ambapo kila kilo 1 ya mbegu za ngano nilinunua kwa shilingi 2,000/=.Ingawaaje kwa maeneo mengine zinauzwa kwa kati ya sh. 1,000 hadi sh 1,500 kwa kilo.
Kama ningenunua chakula cha kawaida kilichochanganywa ningelinunua kwa sh. 700 kwa kilo hivyo kwa hizo kilo 16 ningetumia kiasi cha sh. 11,200/= kwa siku.

Kwa matumizi ya hydroponic fodder nimeweza kuokoa kiasi  sawa na sh. 7,200/= kwa chakula cha  kila kuku 106.

Kwa kuku wangu 350 huwa wanatumia takribani kilo 50 kwa siku ambazo hunigharimu sh. 35,000 kila siku ila kwa kutumia hydroponic  fodder ninaweza kutumia kiasi cha sh.13,200 kwa siku ambapo ninaokoa kiasi cha sh. 21,700 kila siku.


UPATIKANAJI WA CHAKULA KWA MUDA WOTE
Ili uweze kuhakikisha chakula cha njia hii kinakuwa tayari kwa malisho ya kuku wako kila siku lazima ujue mahitaji halisi ya chakula kwa siku moja. Kwa mfano mimi kuku wangu wanatumia kilo 50 kwa siku. Kutokana na matokeo niliyoyapata katka uoteshaji wa mbegu zangu  ya kwamba kilo 2 mbegu zinazalisha kilo 16 za fodder kwa siku 8, je nahitaji mbegu kiasi gani kutengeneza fodder ya kuwatosha kuku wangu wote 350 kwa siku?  Nitachukua kilo 50 gawanya kwa kilo 16 za fodder niliyoipata kutokana na kilo 2 za mbegu, jibu lake litakuwa ni 3.125 na jibu hili nitalizidisha kwa 2 (kiasi cha mbegu kilichozalisha kilo 16) = 6.25 (6.25 ni sawa na kilo za mbegu nitakazotakiwa kuotesha kila siku)
Kwa maana hiyo itanilazimu kupanda kilo 6.25 za mbegu kila siku katika tray kubwa zenye uwezo wa kubeba kilo 6.25 za mbegu. Kama nitatumia tray moja kubwa kupanda mbegu zote hizo itanilazimu niwe na tray 8 za namna hiyo kwa sababu nitakuwa napanda mbegu kwenye tray kwa kupishanisha siku moja moja kwa maisha yangu yote ya ufugaji na kila tray inapovunwa inasafishwa na kupandwa mbegu zingine siku hiyo hiyo.
Maoni:
Iwapo utaamua kutumia njia hii kama chakula cha kuku ni vizuri pia kuwapa kuku punje kavu au mapumba matupu kwa uwiano wa 2 kwa 10 ili kuhakikishwa kwamba mmengenyo wa chakula unafanyika vizuri pasipo kuleta hatari ya constipation na siyo lazima kufanya hivyo kila siku. Virutubisho vilivyo kwenye fodder ya ngano au fodder ya shairi ni vya kutosha kabisa kwa mahitaji ya kuku wako.
Ukitumia shairi ni bora zaidi kwa sababu ina ukuaji wa haraka sana zaidi ya mara mbili ya ukuaji wa ngano, lakini fodder ya ngano inapendwa zaidi na kuku kuliko fodder ya shairi kama ukiwapa zote kwa pamoja watashambulia zaidi ngano kabla ya kuhamia kwenye shairi.

KUPUNGUZA GHARAMA
Tukitaka kupunguza gharama kwa asilimia kubwa Zaidi nilijaribu kufanya upelelezi mdogo kuhusu badala ya kununua mbegu za ngano au shairi kwa watu kwanini nisilime mwenyewe kwasababu ni kazi endelevu na ndio naitegemea kwa malisho ya kuku wangu.
Zao la Ngano linachukua siku 4 hadi siku 5 kufanya germination. Na seed life ni hata miaka 30. Siku zitakazohitajika mpaka uvunaji ni 120 days.
Zao la Shairi linaanza germination kuanzia siku ya 1 hadi siku ya pili kupandwa ( 34F to 36F) ,na seed life ni miaka 2. Siku zitakazohitajika mpaka uvunaji ni 40-55 days. Ninatumai kuwa mmelifurahia somo hili.

Imeandaliwa na Michael Ngonyani
                                

5 comments:

Anonymous said...

Nimefurahia sanaa somo hili la hydroponics fodder. Shukrani sanaa Mr. Michael.
So, sprayer ndo kwa ajili ya umwagiliaji?
and,
Hizo tray special ni wapi zinapatikana?

Anonymous said...

Swali Jingine please.
Mizizi ya hizo fodder hujishika kwenye nini, vile hatutumii udongo?
Pia, Je zile siku mbili Kabla ya kuweka sehemu ya hewa safi, ni wapi tunaweka tray zetu kungoja kuchipua?

FREBU SPORTS said...

Mtaalamu je ni mbolea gani twatumia kuzalishia Ngano au Shayiri au ukiweka katika maji basi umeshamaliza kazi?

Na je twaweza kuja kwako kupata darasa?

Anonymous said...

Mdau somo zuri limeeleweka sana. ubarikiwe!
swali shairi/ ngano hizo nafaka zinapatikana sokoni
soko gani naweza kuzipata.

kuna mdau kauliza kuhusu mbolea. nijuavyo Mimi mbolea ipo ila sio lazima iwekwe hata bila mbolea mmea utakuwa bora kwa kulishia mifugo yako.

FREBU SPORTS said...

Kuna maswali hapo sijaona majibu yake jamani