Somo na Mohamed.
Vitunguu ni moja ya zao la bustani linalopendwa na kutumiwa
kwa wingi sana si hapa nchini tu bali duniani kote kwa ujumla. Linachukua
nafasi ya pili baada ya nyanya. Kitunguu kinatumika katika kachumbari, kama
kiungo kwenye kitoweo kama vile Samaki, nyama, mboga za mahani n.k. Majani ya
vitunguu hutumika kama mboga. Vitnguu pia hutumika kuandalia supu.
MAHITAJI MUHIMU KATIKA UZALISHAJI WA ZAO LA VITUNGUU.
Vitunguu hustawi maeneo yasiyo na mvua nyingi sana, yenye
baridi kiasi wakati wa kiangazi na maeneo yasiyo na joto kali pamoja na ufukuto
wa ukungu wakati wa kukomaa kwa vitunguu.Vitunguu hustawi vizuri kwenye udongo
wenye rutuba ya kutosha, unaoruhusu mizizi kupenya na unaohifadhi unyevu kama
vile udongo wa nusu mfinyanzi nusu tifutifu.
UPANDAJI WA MBEGU ZA VITUNGUU.
Hapa kwetu Tanzania upandaji huanza mwezi March hadi Mei
kutegemea na msimu wa kilimo ulivyo. Hivyo kilimo hiki huanza mara baada ya
mvua kubwa za masika kumalizika. Kipindi cha kiangazi na baridi huruhusu ukuaji
mzuri wa vitunguu.Mbegu za vitunguu huoteshwa mapema katika kitalu. Mbegu
zinaweza kutawanywa au kupandwa kwa mistari katika tuta la kitalu. Katika
upandaji wa mstari mbegu hupandwa katika nafasi ya sm 10 hadi 15 kati ya mstari
na mstari.Baada ya kupanda mbegu hufunikwa na udongo mwepesi na baadaye
matandazo juu ya tuta. Mara baada ya mbegu kuota matandazo yaondolewe na badala
yake kichanja cha nyasi kijengwe ili kuiwekea kivuli miche michanga. Mbegu za
vitunguu huota baada ya siku 7 hadi 10.
KUPANDIKIZA MICHE BUSTANINI
Upandikizaji wa miche ya vitunguu hufanyika baada ya miche
kukua na kufikia unene wa Penseli. Mara nyingi miche hii hukaa kwenye kitalu
kwa siku 40 baada ya kupandwa.Usichelewe kuhamishia miche yako bustanini maana
ukipandikiza miche mikubwa itaanza kutoa majani badala ya kitunguu (bulbs).
Hivyo mara nyingi miche ya namna hii hubaki na suke la maua.Wakati wa
kupandikiza usikate wala kupunguza majani. Miche ipandikizwe sm 30 kati ya
mstari na mstari na sm 10 kati ya mche na mche.Upandaji katika bustani
hufanyika kwenye mistari katika matuta au kwenye vijaruba. Vijaruba hutumika
katika maeneo tambarare na yenye ukame ili kuhifadhi unyevu baada ya kumwagilia.
Sehemu zenye udongo mzito na wenye maji mengi tumia matuta yenye mwinuko wa sm
10 hadi sm 15 kutoka usawa wa ardhi.
MATUNZO YA BUSTANI YA VITUNGUU.
Umwagiliaji
Zao la vitunguu linahitaji maji katika kipindi chote cha
ukuaji wa mmea na hasa wakati wa utungaji wa tunguu (bulb).Katika kipindi
kisicho na mvua, miezi ya mei hadi Agost, umwagiliaji ufanyike mara moja kwa
wiki.Ili kuharakisha kukomaa kwa vitunguu, unashauriwa kupunguza kiasi cha maji
kadri vitunguu vinapoendelea kukua. Pia ni vema uache kumwagilia maji wiki nne
hadi sita kabla ya kuvuna. Kwani muda kamili wa kukomaa vitunguu na kuvuna ni
siku 90 hadi 120 kutegemeana na aina ya mbegu.
KUDHIBITI MAGUGU NA KUPANDISHIA UDONGO.
Kitunguu ni zao lisiloweza kuvumilia magugu, magugu
husababisha kupungua kwa ukubwa wa kitunguu, hueneza magonjwa na husababisha
kudumaa kwa kitunguu.Katika bustani ya vitunguu, magugu yanaweza kung'olewa kwa
kutumia jembe dogo la mkono, kung'olea kwa mkono au kwa kutumia madawa ya
kuulia magugu (herbicides).
Note: Unapotifulia, epuka kutifua kwa kina kirefu maana
utaharibu udongo na vitunguu vyenyewe kwa kuwa mizizi ya vitunguu ipo juu juu
sana.
Kupandishia udongo kwenye mashina ya vitunguu ni hatua
muhimu ili vitunguu visiunguzwe na jua. Hakikisha kwamba mashina ya vitunguu
vyako yako ndani walau sm 5. Pia kuna aina nyingine ya vitunguu ambavyo hutoa
au hupandisha tunguu lake juu ya udongo vinapokua. Hivyo kupandishia udongo ili
kufunika tunguu ni muhimu sana.
MAGONJWA NA WADUDU WAHARIBIFU.
Wadudu waharibifu.Kuna aina tatu za wadudu wanaoharibu hili
zao;
1. Viroboto wa vitunguu,Hawa ni wadudu waharibifu namba moja
wa zao vitunguu hapa nchini kwetu Tanzania. Husababisha upotevu mkubwa wakati
wa mavuno. Wadudu hawa huonekana hasa kipindi cha joto.
Dalili.
Majani yaliyoshambuliwa na wadudu hawa huwa na mabaka meupe
yenye kung'aa. Katika hali iliyokithiri majani yote huwa na tabaka jeupe au
kijivu na baadaye hunyauka kabisa.
Kuzuia.
Mdudu huyu huzuiwa kwa kupiga dawa ya kuulia wadudu
(insecticide) kama vile Marathion, Thiodan-35, ParathionIli kupunguza uvamizi
mkubwa panga kupanda vitunguu mapema ili kipindi cha joto kinapofika kikute
vitunguu vyako vimekomaa.Epuka kupanda vitunguu katika shamba lililokuwa
limepandwa jamii ya vitunguu hapo kabla kama vile liksi, vitunguu swaumu, n.k.
2. Funza.
Mdudu huyu huathiri kitunguu kwa kukata miche na minyoo wa
vitunguu.Hawa huzuiwa kwa kuzingatia mzunguko wa mazao.
MAGONJWA.
1. Ukungu mweupe.Ugonjwa huu huonekana wakati wa baridi
ulioambatana na unyevu mwingi angani.
Dalili.
* Utaona unga unga wa rangi ya zambarau katika majani.
* Majani hugeuka rangi na kuwa ya njano na kisha hunyauka.
* Ugonjwa huu hupenya hadi chini kwenye tunguu na
husababisha kuoza.
KUZUIA
Fanya kilimo cha mzunguko ukihakikisha unapanda mazao
mengine yasiyo jamii ya vitunguu. Panda vitunguu tena baada ya miaka mitatu
kama athari ilikuwa kubwa.Tumia dawa za ukungu (fungicides) kunyunyizia katika
shamba. Hii ifanyike kabla ya dalili kuonekana. Tumia dawa kama Zineb ya unga,
Maneb, Dithane M45, n.k.Wakati unapoona dalili za hali ya hewa yenye baridi
ikiambatana unyevunyevu angani. Katika kipindi hiki piga dawa kila baada ya
siku sita ili kuzuia ugonjwa kuingia.Ugonjwa ukishaingia kwenye mmea hauzuiliki
kwani hakuna dawa ya kuponesha.
2. Ukungu wa kahawia.
Ugonjwa huu huleta madhara makubwa wakati vitunguu vikiwa
bustanini na hata wakati vitunguu viko ghalani.
Dalili.
Vikovu mbonyeo hujitokeza kwenye majani na baadaye huwa na
rangi ya zambarau. Vikovu hivi hukua na kutengeneza vidonda ambavyo hukua na
kufanya mzunguko katika jani zima au katika shina la kitunguu. Baada ya wiki
kama tatu tangu kuingia kwa ugonjwa huu, majani yote huanguka na kidmsha
kukauka.Ugonjwa huu hushambulia kitunguu hata baada ya kuvuna kupitia sehemu ya
shingo ya kitunguu au sehemu yoyote yenye kovu, kidonda au mkwaruzo.
NAMNA YA KUZUIA
*Katika bustani, unapoona kitunguu kina dalili ya ugonjwa
huu, ng'oa na choma.
* Kwa kinga ya bustani, piga dawa za Dithane M45 na dawa
zingine za ukungu. Dawa hizi hupunguza uwezekano wa kuenea kwa ugonjwa huu.
* Tumia kilimo cha mzunguko wa mazao katika eneo la bustani
yako. Usipande vitunguu katika mzunguko wa jamii ya vitunguu.
* Wakati wa kuvuna epuka kukata vitunguu na kusababisha
vidonda na makovu.
* Ukishavuna anika kwa siku mbili kabla ya kuhifadhi kwenye
magunia.
3. Ugonjwa wa kuoza mizizi
Huu ni ugonjwa unaotoka udongoni na huenezwa na vimelea vya
Ukungu (fungi).DaliliMizizi kugeuka rangi na kuwa njano na kisha zambarau.
Baada ya muda ugonjwa huenea na mizizi hufa kwa kunyauka.
KUZUIA
Panda vitunguu kwa mzunguko wa mazao. Epuka kurudia kupanda
vitunguu kwa mfululizo.Panda aina za mbegu zinazostahilimili magonjwa
kama;Excel, L36, Granex, White Granex, Red creole.
UVUNAJI WA VITUNGUU
Kwa ujumla uvunaji wa vitunguu huanza siku 90 hadi 150 tangu
kwa miche kupandwa yaani miezi mitatu hadi mitano tangu kupandikizwa
bustanini.Utagundua kuwa vitunguu vyako viko tayari kuvunwa unapoona karibu 50%
au zaidi ya mazao shambani yanaanguka au majani kukauka.Ili kurahisisha
ukaushaji wa vitunguu, pangilia muda wako ili uvunaji ukutane na kipindi cha
joto na kiangazi.Uvunaji ufanywe kwa kung'oa baada ya kumwagilia maji bustani
siku moja kabla ya kuvina.Baada ya kuvuna, kata majani sm 2 juu na kata mizizi
sm 2 chini. Usikate chini sana ya shingo maana husababisha jeraha na kupelekea
kitunguu kuoza.
Mavuno.
Mavuno ya vitunguu vilivyotunzwa vizuri yaweza kufikia gunia
65 hadi 110 kwa hecta.
Bei ya gunia moja la vitunguu ktk soko zetu Dar es Salaam
imepanda kufikia sh. 140,000 kwa gunia.
Mfano
Ukivuna gunia 100 ni sawa na kuuza kwa(gunia 100 X 140,000 =
14,000,000) kwa ekari.
Shukurani sana kwa Mwanakundi kwa kutuletea somo hili zuri, Tunaomba masomo zaidi mtuletee kupitia Barua pepe yetu: mfumata@gmail.com
2 comments:
Somo zuri, naomba masomo zaidi
INAMAANA MKULIMA UKIWA NA HEKARI 50 ZA VITUNGUU NA UKAVUNA ZOTE UTAPATA KIASI CHA SHILINGI 700,000,000/=
KUNA HAJA YA KUFANYA KILIMO HIKI
Post a Comment